Actualités
Barua ya wazi kwa Mheshimiwa Jakaya Mrisho KIKWETE.
Tarehe 6 Machi 2008
Kutoka
'Taasisisi ya Uongozi'
Mheshimiwa Rais;
Kabla ya yote, tunapenda kuchukua fursa hii ili kutoa salam na pongezi za dhati kwa kuchaguliwa kwenu kuwa Mwenyekiti
wa Umoja wa Afrika na vile vile kutowa mchango mkubwa katika juhudi za kutafuta ufumbuzi katika mgogoro wa kisiasa ulioikumba
nchi ya Kenya tangu desemba 2007.
Mchango wenu Mheshimiwa, pamoja na Waheshimiwa Kofi ANNAN, Rais Mstaafu Benjamin MKAPA, Mheshimiwa Graca MACHEL na viongozi
wengine mashuhuri kutoka Bara la Afrika umekuwa ni kielelezo thabiti kwamba Wana wa Afrika wenyewe wanao uwezo, uzowefu, ujuzi
na mbinu za kutuliza fujo na migogoro inayolikabili bara hili mara kwa mara.
Tunapenda kutowa shukrani zetu za dhati kwa kazi ambayo mmeifanya kwa ufanisi mkubwa na hivyo kuleta matumaini makubwa siyo tu
kwa maslahi ya wananchi wa Kenya, bali kwa Afrika nzima na hata ustawi wa dunia nzima.
Hata hivyo Mheshimiwa, katika eneo hilo, pamoja na juhudi zote zilizotangulia na mchango wa mataifa, bado kuna kero nyingine
kubwa ambayo kwa ufupi inahitaji sasa mchango mpya na ushirikiano wa mataifa. Kero hii inahusu tishio la kutokomea kwa mpango
mzima wa utawala wa kidemokrasia nchini Burundi.
Bila kupoteza muda katika mitazamo tofauti na ya kimalumbano ya wanasiasa nchini humo, ukweli ulio wazi sasa hivi na ambao tunaamini
ni vema ukaarifiwa kwenu Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika, ni kama huu ufwatao:
1. Tangu kuanza kwa awamu ya utawala wa kidemokrasia , sasa ni miaka miwili mfululizo vyombo muhimu vya utawala vikiwa vimekwamishwa
na kushindwa kutekeleza wajibu wake wa kikatiba na kisheria. Imani ya msingi kati ya vyombo vya utekelezaji (Executive) na vile vya
usimamiaji sheria (bunge) imetoweka. Hofu kubwa inazidi kutanda miongoni mwa raia wa Burundi;
2. Kumekuwa na vitendo vya uvunjaji wa amani na utulivu katika pembe zote za nchi na hisia ya ya kusingizia kwamba vinaendeshwa na
wapiganaji wa FNL haikubaliki tena, maana kuna ushahidi wa kutosha kabisa wa kuhusika moja kwa moja kwa vyombo vya dola na taasisi
za usalama (majeshi na wapelelezi wa serikali).
3. Vitisho dhidi ya utawala wa sheria na wa demkrasia vimezidi kutanda hasa kutokana na serikali kushindwa kabisa kuendesha na kusimamia
mabadiliko na mageuzi muhimu kama ilivyoagizwa na maazimio makubwa yakiwemo Makubaliano ya Amani ya Arusha, ikiwa ni pamoja na kushindwa
kupanga Kamati ya 'Ukweli na Usuluhisho', marekebisho ya Katiba, sheria na taratibu mpya vya uchaguzi, na kadhalika;
4. Kushindwa kwa serikali kusimamia mpango wa kupokonya silaha mikononi mwa wasioruhusiwa kuzimiliki umeondoa matumaini ya kurejea haraka
kwa usalama na utulivu;
5. Tayari kuna vitishio vinavyoashiria kwamba uchaguzi unaotaotarjiwa mwaka 2010 hautakuwa wa haki na wa wazi, ikiwa hali iliopo sasa hivi
itadumu na kupelekea vurugu katika muda wa maandalizi ya awamu ifwatayo;
6. Misingi ya demokrasia na utawala bora inazidi kutozingatiwa siku hadi siku: kuzuka kwa kuwatupa jela jela wanasiasa bila sababu za
kisheria wala kuzingatia kanuni, kuteswa, ubadhirifu wa mali ya umma, kutozingatia haki za msingi za binadamu, kutoheshimu vyombo vya
utawala wa kidemokrasia, utegnao na uwiano kati yavyo;
7. Haki binafsi ya kujieleza na kutoa na kutangaza fikra na hata ile ya ya kuishi zinaendelea kuburuzwa na vyombo vya dola, kila kukicha;
8. Serikali inashindwa kufanya kazi kufwatia mikwamo itokanayo na kuendeleza malumbano ya ndani ya chama tawala, hali amabayo inapelekea
kujiuliza kuhusuu uwezo wa viongozi wa ngazi za juu kushughulikia maswala ya kitaifa na ya maendeleo ya jamii, ikiwa ni pamoja na maswala
ya mshikamano na usalama wa raia.
9. Waraka wa hapa majuzi kutoka kwa Wabunge wa Burundi kumpelekea Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ni kielelezo tosha cha vurumai ya kisisasa
inayoendelea kuikumba nchi ya Burundi. Hoja hizo nzito nzito zilizoelezwa kwa uwazi zinatosha kabisa kuyafanya mataifa kuona umuhimu wa
kuingilia kati swala hili kabla halijawa sugu na kusababisha madhara zaidi.
Kwa misingi yote hiyo, tungependa kukuarifi Mheshimiwa kwamba juhudi zote zilizoendeshwa kwa jasho, moyo na kujituma kwa Tanzania na wananchi
wake, wakishirikiana na mataifa kadhaa katika eneo letu na mataifa mengine kwa ujumla zimekuwa hatarini kuyoyoma iwapo nchi ya Burundi
itaachiliwa bila kurejeshwa katika mstari wa Demokrasia na Utawala Bora.
Katika hali hii, tungependa kukuomba Mheshimiwa haya yafwatayo:
- Kuagiza ujumbe maalum wa Umoja wa Afrika kuja nchini Burundi , ambao ukiongozwa na Kiongozi mashuhuri wa Kiafrika utaweza kuanzisha
mazungumzo kati ya kambi za wanasiasa wa Burundi na kujionea hali halisi amabyo kama haikudhibitiwa inaweza kuielekeza nchi ya Burundi
moja kwa moja katika vita;
- Ujumbe huo utowe maamuzi ambayo yatashinikizwa kwa tamko na azimio la Umoja wa Afrika na Umoja wa Mataifa ili kuwahimiza viongozi wa
ngazi zote kutekeleza maamuzi hayo;
- Kuhakikisha kwamba mipango na maadalizi ya uchaguzi wa mwaka 2010 vinasimamiwa na Umoja wa Afrika, pamoja na taasisi binafsi na huru
za kimataifa: maana inaonekana kwamba mahesabu ya uchaguzi wa mwaka 2010 ni moja ya agenda inayosababisha kuharibika kwa hali ya lkisiasa
na usalama sasa hivi;
- Kuendeleza juhudi za Tanzania katika kutafuta ufumbuzi wa swala la FLN. Tungeomba tena Mheshimiwa Rais mweze kuhakikisha tena binafsi,
makubaliano ya kumaliza mapigano (cease-fire) kati ya majeshi ya serikali na wapiganaji wa PALIPEHUTU FLN yanahakikishwa kwa kutekelezwa
kikamilifu, ili raia wasio na hatia wasiendelee kuuliwa katika vita hivi visivyo na sababu, msingi wala manufaa kwa yeyote.
Mheshimiwa Rais;
Tunaamini kwamba mchango wenu katika swala la Burundi ni mkubwa na bado unahitajika hadi leo na kuingilia kwenu binafsi katika swala hili
kunaweza kukarejesha matumaini ya utulivu katika eneo hili la Afrika.
Kwa uzowefu wenu na hadhi yenu, ni matumaini yetu kwamba Historia itakumbuka na kuenzi juhudi zenu kama kiongozi wa Afrika ambae amejitolea
kwa hali na hadhi ili kuokoa demokrasia changa nchini Burundi.
Burundi Transparence
 |